Huduma ya Majitaka

Mtandao wa Majitaka ni nini?

Mtandao wa majitaka ni mfumo au ni bomba linalopita katika sehemu mbalimbali za mitaa/ makazi ya watu kwa ajili ya kukusanya maji yaliyotumika na kuyasafirisha kwenda maeneo yaliyotengwa. Maji yaliyotumika yanaweza kuwa ni maji toka chooni, bafuni, maji yaliyooshea vyombo, maji yaliyopigia deki, yaliyofulia n.k ambayo si safi na salama.

FAIDA ZA KUJIUNGA NA MTANDAO WA MAJITAKA

Kinga ya maradhi/magonjwa ya mlipuko

Majitaka yote yatakuwa yanaondoshwa moja kwa moja kupitia bomba la majitaka, hivyo hatutegemei kuwepo kwa magonjwa kama ya kipindupindu na malaria ambayo huletwa na mazalia ya Inzi na Mbu.

Hakuna gharama ya kuchimba choo

Endapo utajiunga na mtandao wa majitaka hutakuwa na sababu ya kuchimba choo cha shimo, hivyo utakuwa umeokoa fedha nyingi za uchimbaji na ujenzi wa choo.

Paa/Bati halitaharibika

Nyumba nyingi zenye vyoo vya shimo mapaa (mabati) yameharibika na kutoboka kutokana na mvuke wa kinyesi cha chooni, kwa hivyo basi ili kuepukana na kufanya matengenezo ya mara kwa mara ya bati ni vyema ukajiunga na mtandao wa majitaka.

Kutojitokeza kwa harufu mbaya nyumbani

Mara nyingi vyoo vya shimo hutoa harufu mbaya kwa sababu kinyesi hubaki palepale ndani ya shimo, pia ili nyumba yako isizungukwe na harufu mbaya ni vyema uchafu wako ukasafirishwa moja kwa moja kupitia kwenye bomba la majitaka.

Kuepuka kutumbukia

Watu wengi waliojenga vyoo vya shimo ambavyo sio imara huatarisha maisha yao kwa kutumbukia endapo choo cha shimo kitatitia.

HUDUMA YA MAJITAKA

Mamlaka imelaza mabomba ya Majitaka yenye urefu wa km 105 katika maeneo ya Uhindini, Sokomatola, Majengo, Jacaranda, Mbalizi road, Forest mpya, Block T, Mwanjelwa, Simike juu, Simike Senjele, Itiji, Kalobe Iyunga MTC, Viwandani Isanga Uzunguni na Ilolo

Mamlaka huyakusanya majitaka yote kwa wateja waliojiunga na mtandao wa majitaka na kuyapeleka kwenye Malambo yaliyopo eneo la Kalobe kwa ajili ya kutibiwa na baadae huruhusiwa kuingia mtoni.

NAMANA YA KUJIUNGA NA MAJITAKA

Kwa wateja ambao tayari wameshaunganishwa na huduma ya Majisafi, wanatakiwa kuja ofisini kuomba kuunganishwa na huduma hii, kisha mafundi wetu watakwenda kupima na kuandaa gharama kulingana na eneo husika. Kisha mteja atatakiwa kulipia hizo gharama na kuunganishwa katika mfumo huu.

Kwa wale ambao bado hawajaunganishwa, watalazimika kufuata taratibu za kuomba uanachama mpya. Ambazo zinapatika hapa.